MAWAZIRI WATAJWA KUFICHA MABILIONI BENKI ZA USWIZI
ZITTO ASEMA YUMO KIONGOZI WA JUU WA SERIKALI YA SASA,WENGINE NI WA AWAMU YA MKAPA, ATISHIA KUWAANIKA
Waziri Kuvuli wa Fedha Zitto Kabwe wa Kambi ya Upinzani,akiwakilisha
bajeti mbadala ya kambi hiyo Bungeni Dodoma jana.
TUHUMA kwamba baadhi ya vigogo Serikali wameficha mabilioni ya fedha
nchini Uswisi jana ziliibuka tena bungeni, huku Kambi ya Upinzani ikidai
kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa
Serikali haitawataja.
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto
Kabwe aliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na wafanyabiashara
wakubwa walioficha Sh315.5 bilioni nchini Uswisi, akisema kwamba watu
hao “wanafahamika”.
Juni mwaka huu, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa
taarifa inayoonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa
Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na
wafanyabiashara.
Akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi bungeni jana, Zitto
ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo alisema mmoja wa viongozi wa
juu wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa Serikali za awamu zilizopita ni
miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo.
“Kambi ya Upinzani bungeni
imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na
baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni mwa fedha hizi,”
alisema Zitto.
Pia aliitaka Serikali kuliambia taifa ni hatua
gani itakazochukua kurejesha fedha hizo pia kuwataka wamiliki wake na
kama ikishindwa, wao watawataja.
“Tunaitaka Serikali kutoa
taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka
Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya
watu wenye umiliki wa fedha hizo iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi,”
alisisitiza.
Fedha hizo zinadaiwa kutokana na biashara
(deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye
Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na
kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara
zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Baada ya Zitto
kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher
Ole-Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo.
Sendeka
alisema Zitto alisema miongoni mwa walioficha fedha hizo ni kiongozi wa
juu wa Tanzania, lakini akashangaa Serikali kutohoji juu ya kauli hiyo.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, mheshimiwa Zitto amewatuhumu viongozi wa Serikali na
kiongozi wa juu kabisa kuwa wameficha fedha Uswisi,” alisema.
Alisema,
lakini pamoja na tuhuma hizo, hakuna kiongozi wa Serikali aliyesimama
na kutolea ufafanuzi hivyo akaomba mwongozi ili Zitto aruhusiwe
kuwataja.
Sendeka alisema tuhuma hizo ni nzito na zimeichafua
sura ya Serikali hivyo ni vyema ijulikane ni nani kati ya Serikali na
Zitto atabeba mzigo wa kuwataja.
Naibu Spika, Job Ndugai alisema
angetoa mwongozo huo baada ya kuipitia hotuba hiyo ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni na kuona kama ina matatizo. Hata hivyo, hakutoa
mwongozo huo.
Oxford wabanwa
Wakati huohuo, kambi hiyo rasmi
ya upinzani imeitaka Serikali kuinyang’anya Kampuni ya Oxford University
Press Tanzania (OUPTL), zabuni ya kuchapisha na kusambaza vitabu.
Zitto
alisema kampuni hiyo imejihusisha kuwahonga maofisa wa Serikali katika
kupata zabuni hiyo jambo linaloipotezea sifa kuendelea na zabuni hiyo.
Alisema
Julai 3,2012 Benki ya Dunia ilitangaza kuifungia kampuni hiyo kutokana
na vitendo vya rushwa ambavyo kampuni hiyo ilikiri kuhusika kwake.
Kampuni
hiyo ilishinda zabuni ya kusambaza vitabu nchi za Afrika Mashariki
katika miradi mbalimbali ya elimu iliyokuwa inafadhiliwa na Benki ya
Dunia.
Alisema kampuni hiyo ilikiri kuhusika kuwahonga maofisa
mbalimbali wa Serikali katika zabuni hiyo na kutakiwa kulipa benki hiyo
Dola 500,000 za Marekani.
Kutokana na kukiri kwake huko, Mamlaka
ya Ununuzi ya Umma ilitangaza kuifungia kampuni hiyo hapa nchini kwa
kipindi cha miaka saba.
“Wakati ikifungiwa tayari tulishawapa
zabuni ya kusambaza vitabu vilivyotokana na chenji ya rada ambazo
ziliamuliwa kuwa zitaenda kununua vitabu,” alisema.
Kambi hiyo
imeitaka Serikali kuinyang’anya OUPTL zabuni hiyo ya kusambaza vitabu na
badala yake kazi hiyo zipewe kampuni za ndani ya nchi.
Alisema
tabia ya Serikali kufanya kazi na kampuni ambazo tayari zina dosari za
kifisadi au kukiuka sheria inatoa picha mbaya kwenye uchumi.
Zitto
alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwachukulia hatua
maofisa wote wa wizara waliohusika katika rushwa hiyo ya Oxford.
Ufisadi wa Sh70 bilioni
Katika
hatua nyingine Zitto alisema Serikali inatumia Sh70 bilioni kwa mwaka
kulipa mishahara ya watumishi hewa fedha ambayo ingeweza kutumika
kuwalipa walimu na madaktari na kumaliza migogo iliyopo.
Fedha
hizo zinatosha kulipa mishara ya mwezi mmoja kwa walimu wa ngazi ya
cheti wanaoanza kazi 286, 415 wanaokiwa kulipwa mshahara wa kiwango cha
Sh244,400 kwa mwezi.
Zitto alisema Waziri wa Fedha na Uchumi
alikiri mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi kwamba Februari mwaka huu
Serikali ililipa jumla ya Sh5.1 bilioni zikiwa ni mishahara hewa.
“Hii ina maana kwamba Serikali hutumia zaidi ya Sh70 bilioni kwa mwaka kuwalipa mishahara watumishi hewa,” alisema Zitto.
Alisema
Waziri ausambaratishe mtandao huo wa wezi ili fedha wanazolipwa
watumishi hewa zitumike kuwalipa walimu na madaktari kwa kuwa fedha hizo
zinatosha kabisa kwa kazi hiyo.
“Siku zote Serikali imekuwa
haitimizi matakwa ya wafanyakazi hasa kwenye sekta za afya na elimu kwa
madai kwamba Serikali haina fedha wakati mabilioni hayo yanatumika
kuwalipa watu wasiofanya kazi,” alisema Zitto.
Akirejea taarifa
ya Waziri wa Fedha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi ya
Agosti 7, 2012, Zitto alisema uhakiki wa watumishi hewa uliofanyika
Januari 2012 na kubaini majina 9,949 ya watumishi hewa kwenye
halmashauri 133 na taasisi za Serikali 154.
“Idadi hii ya
watumishi hewa ni sawa na idadi ya watumishi walioajiriwa katika sekta
nzima ya madini kwenye migodi ya dhahabu hapa nchini,” alisema Zitto.
Alisema
watumishi hewa wanaokaribia 10,000 ni wengi na inaonyesha dhahiri namna
Serikali isivyo makini katika suala ambalo linasababisha upotevu mkubwa
wa fedha za umma.
Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali ya Machi 31, 2009/10 inaonyesha kwamba Sh1.8 bilioni
zililipwa kwa watumishi hewa.
Alisema, Waziri wa Fedha agawe
taarifa za uhakiki wa wafanyakazi wa Serikali kwa wabunge na hatua
zilizochukuliwa dhidi ya vinara wa mtandao huo wa watumishi hewa
serikalini.
Sakata la rada
Msemaji wa Kambi ya Upinzania
katika Wizara ya Fedha, Zitto amesema mjadala wa rada bado mbichi na
kwamba, Watanzania hawatauzima kwa kufurahia chenji iliyorudishwa na
Waingereza.
Alisema wananchi wanataka kujua ni hasara kiasi gani
imepatikana na hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya waliolitia
hasara taifa.
“Umma unataka kufahamu ufisadi huu wa kimataifa
umesababisha hasara gani na hatua stahiki za kisheria zilizochukuliwa
dhidi ya wote walioliingizia taifa hasara,” alisema.
Msemaji
huyo alisema “ Mjadala wa ununuzi wa rada hauwezi kuisha kwa kufurahia
kurejeshewa chenji tu, mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka
ukweli mtupu uelezwe bayana.”
Alisema fedha za kununulia rada
hiyo ambazo ni Dola za Marekani 40 milioni zilikopwa kutoka Benki ya
Barclays ya Uingereza kwa riba ya asilimia 4.9.
“Kambi ya
Upinzani inataka kufahamu kama mkopo huo umeshalipwa wote na jumla
tulilipa kiasi gani cha fedha ikiwamo riba,” alisema Zitto.
Mafuta yatafuna uchumi
Msemaji
huyo amesema fedha zote za kigeni zinazotokana na mauzo ya dhahabu,
bidhaa za viwandani na korosho zinatumika kuagiza mafuta pekee yake.
Alisema
hali hiyo ni mbaya kwa uchumi wa taifa kwani juhudi zote za taifa
kuongeza mauzo ya nje zinaliwa na uagizaji wa mafuta ambao umepanda
katika siku za hivi karibuni.
Alisema taarifa hiyo inaonyesha
kuwa mauzo ya dhahabu nje kwa mwaka 2011 yalikuwa kiasi cha Dola za
Marekani 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7 ya mauzo yote nje, wakati
mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa viwandani yalikuwa na
jumla ya Dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4 ya mauzo yote ya nje.
Alisema
mauzo ya mazao mbalimbali kama pamba, katani, korosho, chai, kahawa na
mengineyo yalikuwa na thamani ya Dola 761.1 milioni kwa kipindi hicho
cha mwaka 2012.
“Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa umeme wa
dharura ambao umesababisha matumizi makubwa ya mafuta na takwimu
zinaonyesha kuwa Serikali inatumia zaidi ya Sh42 bilioni kila mwezi
kuendesha mitambo ya dharura ya umeme,” alisema Zitto.
Habari imeandaliwa na Paul Lawa


0 comments:
Post a Comment